Rais Magufuli aombwa kubariki maandamano ya kufufua mchakato wa katiba mpya

Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) limemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Magufuli apokee na kuyabariki maandamano ya amani ya kushinikiza kufufua mchakato wa Katiba mpya.
Jukwaa hilo limefikia maamuzi ya kufanya  maandamano hayo ya amani nchi nzima kutokana na makubaliano ya mkutano mkuu wa dharura wa JUKATA uliofanyika Septemba 29 mjini Dodoma ambao pamoja na mambo mengine ulikubaliana kuyafanyia kazi maoni ya wananchi ambayo yamekuwa yakisisitiza kuwapo kwa mchakato wa Katiba mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana (Jumamosi) Mwenyekiti wa JUKATA, Hebron Mwakagenda alisema maandamano hayo ya amani yatafanyika nchi nzima Oktoba 30.
Mwakagenda amesema tayari wamemuandikia barua Rais Magufuli  ya kutaka ayapokee maandamano hayo ya amani wakiwa na ujumbe mahususi kwake.
Akifafanua sababu za kumuomba Rais apokee maandamano hayo ni kumkumbusha kuwa mambo yote mazuri anayoyafanya ikiwamo kupiga vita rushwa, kusimamia matumizi mabaya ya mali za umma, yanaweza yasilete tija na maendeleo endelevu na ya muda mrefu kwa sababu mengi yanakosa msingi wa kikatiba.
Akumbuke kuwa yeye siyo Rais wa kudumu, kama asipojenga mifumo imara anayefuata anaweza kuyafuta kirahisi masuala yote mazuri na kuirudisha nchi kwenye hali mbaya kama ambavyo amekuwa akidai. Katiba ndiyo suluhisho la kulinda mazuri yote anayoyafanya na kujenga mifumo thabiti isiyoruhusu nchi kuchezewa na watu wachache kwa manufaa yao,” amesema Mwakagenda huku akielezea umuhimu wa katiba bora kwa nchi kwa kuoanisha na maendeleo.
Imethibitika bila shaka,  nchi zenye Katiba bora ustawi wa Taifa huwa wa hali ya juu kuliko nchi zilizokuwa na migogoro kutokana na kukosa Katiba zenye misingi ya uongozi,” amesema Mwakagenda.
Mwakagenda amefafanua kuwa  maandamano hayo katika ngazi ya kitaifa yatafanyika jijini Dar es Salaam na yataanzia kwenye ofisi za JUKATA na kumalizikia viwanja vya Mnazi Mmoja.
Hata hivyo, Bw. Mwakagenda amesema JUKATA wameshapeleka taarifa kwa wakuu wa polisi wa Wilaya nchi nzima kuwafahamisha kuhusu maandamano hayo ya amani.
Lengo la taarifa hiyo mikoani ni kuwaomba wakuu wa wilaya ambao ni wawakilishi wa Rais kwenye wilaya husika kuyapokea maandamano hayo ya amani,” amesema Mwakagenda.
Mwakagenda amesema kuwa anaamini maandamano ni njia mojawapo ya wananchi kuwasiliana na viongozi wao ambao wamepewa dhamana ya kuongoza Taifa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi yetu huku akiomba maandamano hayo yawekewe ulinzi wa kutosha na jeshi la polisi.

No comments

All rights are recieved.. Theme images by LonelySnailDesign. Powered by Blogger.